Habari

Baba Yangu Mwema

Mtindo wa Maisha ya Hazrat Fatima Zahra sa (5)

Katika Vita vya Ahzab, pindi Mji Mtukufu wa Madina ulipokuwa umezingirwa, kila mtu aliunga mkono vita ile kwa namna yoyote ile alivyoweza.

Hadhrat Zahra (as) pia alikuwa akitoa sapoti yake kwa kuoka mikate (iliyotumika kama chakula katika uwanja wa vita) na alitoa sehemu kubwa ya msaada kwa chochote kile walichokihitajia Mujahidina.

Katika moja ya masiku ambayo alikuwa amewaandalia watoto wake mkate, hakuweza kabisa yeye na wanae kula mkate huo bila baba yake; Kwa sababu hiyo, aliamua kukimbilia katika uwanja wa kivita alipo baba yake na kumwambia: Eeeh Baba Mpendwa! Nimeoka mkate, lakini sikupata hamu kabisa ya kuula mkate huu bila wewe, nimekuletea mkate huu.

Mtume (s.a.w.w.) alimtizama binti yake kwa upendo na huruma na akasema kwa sauti ya utulivu na ya uchovu: “Hiki ndicho chakula cha kwanza ambacho baba yako ataweka kinywani mwake baada ya siku tatu”.

Wakati wa kutekwa kwa Mji Mtukufu wa Makka (au kuifungua Makka au Fat’hu Makka kulikofanywa na Waislamu wakiongozwa na Nabii wa Kiislamu, Muhammad -s.a.w.w-, Disemba 629 au Januari 630 AD), Sayyidat Fatima (sa) alimtengenezea hema Baba yake Mtukufu, Mtume Muhammad (s.a.w.w.), na kumwandalia maji kwa ajili ya kuosha uso wake kutokana na vumbi (ili lisije kupenya kooni) na kunywa ili kukata kiu yake wakati akiondoka kuelekea katika Msikiti Mtukufu wa Makka.

Mapenzi ya Sayyidat Fatima (sa) kwa Mtume (s.a.w.w) yalikuwa ni ibada. Uhusiano kati ya hawa wawili ulikuwa na nuru ya mbinguni. Daima alikuwa akimwita baba yake kwa kusema: Ee Baba yangu Mpendwa.

Alikuwa akimsadikisha sana Mtume (saww), na alifanya juhudi kubwa katika kuhifadhi hadith za Mtume (saww).

Siku zote alitanguliza radhi za Mtume wa Mwenyezi Mungu (s.a.w.w) kabla ya radhi yake.

Na mara nyingi alipitisha kugawiwa kwa chakula cha watoto wake, nguo, mapazia, mikufu, na hata bangiliakivitoa  sadaka katika njia ya Mwenyezi Mungu(swt).

Baada ya kifo cha Mtume wa Mwenyezi Mungu, Sayyidat Fatima Zahra (sa) alimkumbuka sana Baba yake.

Moja ya matukio ambayo yalimfanya Sayyidat Fatimah (sa) amkumbuke sana baba yake ni pale kundi la wavamizi na wanyakuzi wa haki za Ahlul-Bayt (pbuh) walipoamua kufanya walivyo.

Katika hoja zao dhidi ya hoja za Sayyidat Fatima (a.s) walishikamana na Hadithi ya uwongo wakidai kwamba: “Baba yako alisema kwamba sisi, kundi la Mitume, haturithi kutoka kwa yeyote, na wala hatuachi urithi baada yetu”.

Fatimah (sa) alilia sana mkabala na shutuma hii isiyo ya haki na akapaza sauti kwenye kaburi la baba yake akisema:

“Baada yako, kumekuwepo na habari na masuala, ambayo yasingelikuwa makubwa kama ungelikuwepo hai.

Tumekupoteza kama nchi iliyonyimwa mvua na watu wako wametawanyika, njoo uone jinsi walivyopotea….

Ulipotuacha na pazia la udongo likazuia baina yetu na wewe, kundi la watu katika umma wako lilifichua  siri za vifuani.

Na kundi la watu wengine walituacha (na kututelekeza) na wakatutendea yasiyostahili, na urithi wetu ukaporwa….

Laiti tungalikufa kabla yako, pindi ulipoondoka kabla vumbi kukuficha chini yake”.

Sayyidat Fatima (sa) daima alikuwa akikumbuka na kusema: Ni jinsi gani Baba yangu ulivyokuwa mwema, na (tizama) ni gani jinsi gani watu hawa walivyokuwa baada yako?!.

Kwa maelezo zaidi rejea:

(Bihar al-Anwar, Juzuu ya 38, uk.202; Sirat Ibn Hisham, Juzuu ya 3, uk.106; Tabaqat Ibn Saad, Juzuu ya 1, uk.400, Mustadrak al-Wasail, Juzuu ya 12, uk.81, Khutba ya Fadak).

Related Articles

Leave a Reply

Back to top button
×